Monday, November 4, 2013

Ugonjwa wa Hemoroid (HAENORRHOIDS) na kutokwa damu njia ya haja kubwa

TATIZO hili hujulikana pia kama ugonjwa wa vifundo katika njia ya haja kubwa. Jina jingine la ugonjwa huu ni bawasili, lakini kwa daktari bingwa wa upasuaji humaanisha matatizo katika mishipa ya damu (veins) katika njia ya haja kubwa (rectum or anus).

Hutokana na kulegea kwa misuli laini ya mishipa hiyo ya damu, hivyo mishipa kutanuka kuliko kawaida na kulegea, kisha kutokeza katika njia ya haja kubwa, ikiambatana na ukuta wa njia hiyo.

Sababu hasa ya kulegea kwa mishipa hiyo haijaweza kueleweka, lakini mabadiliko yafuatayo huchangia kwa kiasi mkikubwa.

•Kupata choo kigumu mara kwa mara

•Kuharisha mara kwa mara

•Kukaa kwa muda mrefu

•Kuwa na uzito mkubwa kuliko inavyotakiwa (BMI>30)

•Kukohoa mara kwa mara

•Uvimbe tumboni

•Kuzaa watoto wenye uzito mkubwa mfano zaidi ya kilo 4

Dalili

Kuhisi kushuka kwa fundo la sehemu ya haja kubwa wakati wa kupata choo, ambalo linaweza kurudi lenyewe ndani, baada ya kupata choo au inabidi kulirudisha kwa kidole au kushindikana kabisa kurudishwa kidole na kubaki likininng’inia nje kwa muda mrefu.

Kutokwa damu wakati wa haja kubwa ambayo huweza kuchafua nduo za ndani, wakati mwingine damu hutoka kwa wingi na mfululizo bila kuganda, hivyo kuhatarisha maisha.

Kuchafua nguo za ndani kutokana na kutokwa na majimaji sehemu za hajakubwa

Dalili nyingine ni kupatwa na maumivu makali sehemu za hajakubwa, fundo kuwa kubwa sana na kubadilika rangi, wakati damu inapokuwa imeganda ndani ya mishipa yake (thombosed prolapsed haemorrhoids)

Uchunguzi na matibabu

Ni vyema uonapo dalili hizo hapo juu uende katika hospitali iliyo karibu na kupata ushauri na matibabu ya kitaalamu zaidi.

Ni rahisi zaidi kwa daktari kuchunguza na mara moja kugundua ugojwa huu na ukubwa wa tatizo, pia kupanga njia ya matibabu. Pia lazima kuanza na vipimo vya mwanzo, mfano kupima wingi wa damu, (hemoglobin level)

Vipimo kama proctoscopy (kuchuguza kwa chombo maalumu chenye mwanga), proctosigmoidoscopy huweza kufanyika, pia kuwekewa dawa maalumu, kisha kupiga ex-ray (barium enema)

Kwa watu walio na umri mkubwa, mfano miaka 50 na zaidi ni muhimu kuchunguzwa kitaalamu zaidi, maana kundi hili lina hatari ya kupata saratani ya njia ya haja kubwa.

Hivyo, mtu anaweza kufikiri ni tatizo dogo, kumbe anasumbuliwa na saratani ya njia ya haja kubwa na hivyo matibabu hubadilika.

Ugojwa huu pia unaweza kuchanganywa na wa kushuka kwa sehemu ya utumbo na kutokeza nje ya njia ya haja kubwa (rectal prolapsed)

Matibabu

Iwapo hemoroid hazijawa kubwa sana, yaani zipo katika hatua ya kwanza au ya pili hivi, basi ni muhimu kukwepa au kutibu visababishi vinavyochochea ugonjwa kama vilivyoainishwa hapo juu. Mfano choo kigumu na kadhalika. Pia mgonjwa huweza kupewa dawa ya kulainisha sehemu ya haja kubwa.

Iwapo tatizo ni kubwa yaani lipo katika hatua ya tatu au ya nne, au matibabu tajwa hapo juu yameshindikana, basi upasuaji ndiyo matibabu sahihi ya ugonjwa huu. Upasuaji mzuri huo upo wa aina nyingi, mfano kukata au kuvifunga vifundo kwa mpira maalumu. Ifahamike kwamba mgonjwa anapokuja katika hali hatarishi kama vile vifundo kuwa na maumivu makali na kutoka damu kwa wingi (thombosed and prolapsed hemorrhoids), basi huhitajika kufanyiwa upasuaji mapema ili kumwokoa mgojwa.

Matatizo yatokanayo na ugonjwa huu

Yapo mengi, lakini kwa uchache ni kama;

•Kushindwa kupata haja kubwa katika hali ya kawaida kutokana na kupata maumivu

•Choo kuwa kigumu zaidi jinsi muda unavyokwenda na hivyo kuongeza ukubwa wa tatizo

•Kutokwa damu wakati wa kujisaidia haja kubwa

•Kutokwa damu nyingi pale hemoroidi zainapopasuka hivyo kuhatarisha maisha ya mgonjwa

•Kuchafua nguo na kuleta adha katika jumuiya mfano kazini na majirani.

Kwa Mawasiliano 0754310407 

http://www.mwananchi.co.tz/Makala/-/1597592/1691234/-/item/0/-/h54mot/-/index.html

No comments:

Post a Comment