Monday, November 4, 2013

Mambo Muhimu Ya Kufahamu Kuhusu Ukimwi

Maana ya Neno UKIMWI 

Neno UKIMWI ni kifupisho cha maneno Upungufu wa Kinga Mwilini. UKIMWI ni mkusanyiko wa magonjwa yanayotokana na kudhoofika kwa nguvu ya mwili kujikinga na magonjwa kunakosababishwa na Virusi Vya UKIMWI (VVU). 

Maana ya neno Virusi Vya UKIMWI (VVU)

Virusi Vya UKIMWI (VVU) ni vimelea vidogo vidogo vinavyodhoofisha na kufanya mwili kupoteza uwezo wa kupambana na magonjwa. Kawaida miili yetu hukingwa dhidi ya maradhi na chembechembe nyeupe za damu, lakini VVU vikiingia mwilini hushambulia chembechembe hizo na kuzipunguza. Hivyo, mwili ulioingiliwa na VVU hupungukiwa sana na chembechembe nyeupe na hukosa kinga dhidi ya maradhi. Ingawaje mara nyingi maneno haya yamekuwa yakitumika pamoja, ieleweke kwamba yana maana tofauti.

Jinsi Virusi Vya UKIMWI Vinavyoambukizwa 

Virusi Vya UKIMWI vinapatikana katika damu na majimaji mbalimbali yanayotoka kwenye mwili na viungo vya uzazi vya wanawake na wanaume wenye uambukizo. Njia kuu ya kueneza virusi hivi, hasa katika Bara la Afrika ni kujamiiana kusiko salama. Njia nyingine ni kutoka kwa mama mjamzito
mwenye Virusi Vya Ukimwi kumwambukiza mtoto wakati akiwa tumboni, anapozaliwa au wakati wa kumyonyesha. VVU pia huambukizwa kwa kuongezewa damu yenye virusi hivyo. Pia ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kwa kuchangia vifaa vyenye mabaki ya damu kama sindano, mikasi, wembe, mipira ya kutolea mkojo au vifaa vya kutogea masikio. 

Njia zifuatazo haziambukizi VVU 

  • Kushikana mikono na mtu mwenye VVU 
  • Kubadilishana nguo na mtu mwenye VVU ili mradi hazina majimaji au damu kutoka kwa mgonjwa wa UKIMWI 
  • Kuishi pamoja na mtu mwenye VVU 
  • Kushiriki kula chakula pamoja na mtu mwenye VVU 
  • Kugusana au kukumbatiana na mtu mwenye VVU 
  • Kushirikiana bafu na mtu mwenye VVU  
  • Kuumwa na mbu, viroboto, au wadudu wengine. 

Njia hizo zilizoorodheshwa hapo juu zisihusishe damu au majimaii mengine kutoka kwa mgonjwa wa UKIMWI 

Dalili za UKIMWI  

Hakuna njia ya hakika ya kumtambua mtu aliyeambukizwa VVU zaidi ya vipimo vya maabara. Watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI wanaweza kuonekana wazima na wasionyeshe dalili zozote za ugonjwa.  Hata hivyo pamoja na kutokuonyesha dalili zozote, mtu huyu mwenye virusi anaweza akaambukiza watu wengine ikiwa atakuwa na mahusiano yasiyo salama. 

UKIMWI ni hatua ya mwisho ya maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.  Hatua hii ikifikiwa mwathirika huanza kushambuliwa na magonjwa mbalimbali yaitwayo magonjwa nyemelezi Dalili za UKIMWI zimegawanyika katika makundi mawili makuu:

Dalili kuu za UKIMWI 

•Kupungua uzito asilimia 10 au zaidi katika mwezi mmoja, bila sababu inayoeleweka 
•Kuharisha kwa muda mrefu  (mwezi mmoja au zaidi) 
•Homa kwa mwezi mmoja au zaidi

Dalili Ndogo za UKIMWI Utando mweupe mdomoni

•Kikohozi kwa muda wa mwezi mmoja au zaidi 
•Kupata mkanda wa jeshi (moto wa Mungu)
•Vipele sugu na vyenye kuwasha hasa mikononi na miguuni

Mgonjwa akiwa na dalili kuu tatu, au mbili kuu na ndogo mbili uwezekano wa kuwa na UKIMWI ni mkubwa. Hata hivyo vipimo zaidi vya maabara vinahitajika ili kuthibitisha kama mgonjwa ana UKIMWI.

No comments:

Post a Comment