Monday, November 4, 2013

vidonda vya tumbo na matibabu yake

Na Khamisi Ibrahim 

VIDONDA vya tumbo ni uharibifu wa kuta za ndani ya tumbo. Kwa maneno mengine, ni majeraha ndani ya tumbo. 

Vidonda vya tumbo vimegawanyika sehemu mbili; vidonda vya ndani ya tumbo (gastric ulcer) au sehemu ya juu ya utumbo mdogo (duodenal ulcer). 

Vidonda vinavyotokea katika utumbo ndivyo maarufu sana na huonekana zaidi kutokea kwa wanaume, na vidonda vya ndani ya tumbo huwashambulia wote wanaume na wanawake. Kutokana na tafiti za hivi karibuni, takribani mtu mmoja kati ya watu kumi atakuwa na vidonda vya tumbo. 

Vidonda vya tumbo hutokeaje mwilini? 

Chakula kinapoingia tumboni kwa ajili ya kusagwa, tumbo huzalisha majimaji mbalimbali, miongoni mwayo yaliyo muhimu zaidi ni asidi hidrokloriki. 

Asidi hii huanza kula kuta za tumbo/doudeni. Aina zote mbili za vidonda vya tumbo hutokea kutokana na kutolingana nguvu kati ya nguvu ya mnyunyizo wa asidi ya tumbo katika kushambulia na uwezo wa kuta za tumbo katika kuzuia mashambulizi. 

Utokeaji wa vidonda vya tumbo hutegemea zaidi juu ya vipengele viwili. Kwanza, vitu ambavyo huongeza mnyunyizo wa asidi katika tumbo, mfano vyakula vya kusisimua, vyakula vya mafuta, uvutaji wa sigara, utumiaji pombe, chai, kahawa na baadhi ya dawa kama corticostisteroids, caffeine, reseprine, n.k. 

Pili, udhaifu wa ute au kuta za tumbo/duodeni kuzuia ushambuliaji wa asidi. Katika kutibu vidonda vya tumbo, mara nyingi ni lazima kuongeza kinga ya ute au kupunguza uzalishaji wa asidi. 


Mfadhaiko wa akili utokanao na shida za maisha 

Mfadhaiko wa akili utokanao na shida za maisha ni moja ya vipengele vikuu vinavyosababisha vidonda vya tumbo. 

Mfadhaiko huongeza utiririkaji wa asidi ndani ya tumbo. Hii asidi ya ziada ambayo hutiririka ndani ya tumbo imetengenezwa kwa ajili ya kukisaga chakula chochote haraka iwezekanavyo. 

Lakini kama hakuna chakula cha kufanyiwa kazi, asidi hii humomonyoa kuta za tumbo na hivyo kusababisha vidonda. 

Utafiti uliofanywa katika miaka ya hivi karibuni umeonesha kuwa akili hutumia biokemia katika mwili. Baadhi ya madaktari wamesema mfadhaiko huchangakia sana katika kutokeza kwa magonjwa mengi. 

Utafiti wa kisayansi unasema hisia zetu na hali zetu na jinsi tunavyomudu kudhibiti mifadhaiko inaweza kutusaidia kuelewa ni kwa kiwango gani afya zetu zilivyo madhubuti au zilivyo dhaifu. 

Ingawa utafiti katika uwanja huu ni mpya, lakini utendaji kazi wa mfumo wa kinga ya maradhi ya mwili unaweza kukandamizwa na mfadhaiko wa akili/mawazo yatokanayo na shida za maisha. 

Majaribio yaliyofanywa kwa watu wenye mifadhaiko sana kama wajane, wenye kupewa talaka na wenye kupambana na adui yalionesha kuwa watu hao huweza kupata maradhi mara kwa mara kutokana mfumo wao wa kinga ya maradhi kugandamizwa. 

Mfano katika kukabiliana na adui, akili hutambua hofu na ubongo hupata taarifa; neva zenye kujiendesha zenyewe hupanda juu ili kukutana na adui. Hapo moyo huenda mbio, msukumo wa damu nao hupanda na damu huvimba kwenye misuli kwa ajili ya maandalizi ya tendo. 

Oksijeni na virutubishi vingine hukimbilia kwenye ubongo vikimfanya mtu awe hadhiri zaidi, na hapo myunyizo wa adrenalini, homoni yenye nguvu huongezeka. 

Kadiri mfadhaiko unavyokuwa mfupi, ndivyo pia athari yake inavyokuwa fupi. Lakini pindi mfadhaiko unapokuwa mrefu, kama vile kipindi cha ndoa isiyo na amani au katika hali ya matatizo, athari yake huendelea. 

Dalili za mfadhaiko 

Ikiwa bila ya sababu yoyote, zaidi ya dalili sita katika hizi zifuatazo zitatokea, basi mtu amwone daktari kuhusiana na mfadhaiko. 

Kujisikia huzuni sana kiwango cha kutokuwa na matumaini yoyote, kupoteza kabisa uwezo wa akili kufurahi, kupoteza hamu ya tendo la ngono na kupoteza hamu ya chakula (au kula sana). 

Nyingine ni kukosa usingizi (au kulala sana), wasiwasi unaosababisha hali ya kutotulia pamoja, kushindwa falakinika, kushindwa kukumbuka na kushindwa kuamua, kughadhibishwa na vitu vidogo, kujiona huna thamani na kujitenga na marafiki na ndugu. 

Haraka haraka 

Haraka! Haraka! Lazima tufike mahala haraka na turudi haraka! Haraka hizi husababisha vidonda vya tumbo. Mbanano wa ratiba pia husababisha matumbo nayo kubanana. 

Malalamishi makubwa leo ya wagonjwa kwa madaktari wao ni: "Tumbo langu linanisokota na kuniletea matatizo, husikia kiungulia baada ya kula". Haraka na wasiwasi ni baadhi ya sababu ya matatizo haya. 

Tumbo ni kama kioo cha akili. Akili ikihangaishwa, basi wasiwasi na msukosuko wa hisia hufungia breki kwenye viungo vya ndani. Akili iliyohangaishwa na kukimbizwa mbio mbio hupeleka hisia kwenye tumbo na kusababisha mkazo wa ghafla wa misuli na hapo husababisha kiungulia na maumivu. 

Vyakula vya kusisimua 

Vyakula vya kusisimua ni hatari kwa neva za tumbo. Uchunguzi wa kitabibu unabainisha kuwa vyakula vya kusisimua kama vile kachapu, haradali, achali, pilipili na vingine vingi huchangia kwa kiwango fulani kudhuru neva za tumbo na havitakiwi kuliwa hasa kwa mtu mwenye vidonda vya tumbo na mwenye tatizo la kutosagika chakula tumboni. Sababu ni kuwa, visisimuaji huchoma. Tumbo linahitaji kupozwa na si kusasuliwa. 

Dalili za vidonda vya tumbo 

Vidonda vya tumbo huambatana na maumivu ya kuchoma, kuwaka katika sehemu ya juu ya tumbo. Kwa kuwa aina mbili zote za vidonda vya tumbo hutofautiana, ni vizuri zaidi kuelezea kila kimoja. 

(a) Vidonda vya tumboni 

Maumivu ya vidonda vya tumboni mara nyingi hukaa katikati, takribani kati ya nusu ya chini na kwenye kitovu na mara nyingi kula huifanya kuwa mbaya zaidi. Tofauti na maumivu ya vidonda vya utumbo, maumivu ya vidonda vya tumbo mara nyingi hayaishi mara moja pindi yanapoanza. 

(b) Vidonda katika utumbo 

Maumivu ya vidonda vya katika utumbo pia hukaa pale pale (kama katika vidonda vya tumboni). Tofauti na vidonda vya tumboni, katika vidonda vya utumbo mara nyingi kula husaidia kupunguza maumivu. 

Tofauti nyingine ni kuwa, wakati katika vidonda vya tumboni maumivu huongezeka haraka baada ya kula chakula, katika vidonda vya utumbo inaweza kuchukua saa mbili au tatu. Tabia nyingine ya vidonda vya utumbo ni kupotea kwa majuma au hata miezi bila sababu ya wazi. 

Mtu anaweza kulalamika kuwa anapata maumivu baada ya chakula. Hii ni kutokana na msisimko wa mnyunyizo wa asidi ambao hububujika kwenye kidonda. Katika vidonda vya duodeni, huchukua takribani saa mbili hadi tatu ili asidi ifike sehemu ya kidonda. 

Utambuzi wa vidonda vya tumbo 

Utambuzi wa kubainisha vidonda vya tumbo hujumuisha X-Ray. Upimaji wa tumbo na vilivyomo ndani yake unaweza pia kufanywa na njia inayojulikana kama 'endoskopy' au 'biopsy', ambayo huyakinisha hali halisi. 

Matibabu ya vidonda vya tumbo 

Matibabu ya vidonda vya tumbo hujumuisha lishe na kubadilisha mitindo ya maisha na kutumia dawa maalumu. 

Ikiwa matatizo kama kuvuja damu au vitobo sehemu ya kidonda yatatokea, basi hapo upasuaji huwa muhimu. 

Katika vidonda vya tumbo ambavyo ni vikali, matibabu yake hutumia maziwa kwa mwanya wa dakika 15 hadi saa mbili kwa kutegemea ukali wa ugonjwa; kwa wiki moja. Maziwa hutumiwa pamoja na dawa. 

Maziwa si kwamba hupambana na asidi tu, bali pia huchelewesha muda wa tumbo kuruhusu dawa kufanya kazi kwa muda mrefu. Vidonda vya tumbo kwa ujumla hupona ndani ya wiki 4-6 za matibabu. 

Kuzuia mfadhaiko 

Kila mtu ana matatizo na kila mtu hufeli katika mipango yake na kila mtu hupata hasara. Tofauti ni kwamba wakati baadhi ya watu wanaweza kumudu kudhibiti mvurugiko wa mawazo, wengine hawajui kabisa nini cha kufanya na matokeo yake hupatwa na mfadhaiko ambao huweza kuwasabishia maradhi kama vidonda vya tumbo au maradhi ya moyo, n.k. 

Mfadhaiko unaweza kuwa wa muda au wa kudumu. Matokeo yake yana madhara makubwa kama hautadhibitiwa. Ni vipi unaweza kudhibiti mfadhaiko wa akili utokanao na shida za maisha? 

(a) Kuridhika na maisha 

Kama tutakubali kuyapokea maisha kama yanavyokuja, tukaacha kuyakopa maisha ya jana na tukaacha kuhofu maisha ya kesho, hakika kabisa matumbo yetu pia yatatulia. 

Inaelezwa na wataalamu kwamba karibu asilimia 50 ya wafanyabiashara duniani wanasumbuliwa na maradhi ya kutoridhika, kufunga choo, vidonda vya tumbo na maradhi ya moyo. Na wafanyabiashara ambao hawajui namna ya kupambana na wasiwasi au mashaka hufa wakiwa vijana. 

Wasiwasi na hofu ya maisha humfanya yeyote kuwa mgonjwa. Mvurugiko wa hisia una matokeo chanya katika kiwiliwili. Unaweza kuleta ugonjwa ambao ni wa kufisha kama ambao hutokana na lishe dhaifu. Baridi yabisi, maradhi ya moyo, tezi, kisukari, vidonda vya tumbo, kansa, yote yanaweza kusababishwa na mvurugiko wa mawazo. 

(b) Kutopata usingizi wa kutosha 

Ukosefu wa usingizi ni maradhi makubwa katika zama zetu hizi. Haraka na pilikapilika za dunia yetu ya kisasa hazina mfano. Mvurugiko wa mawazo kutokana na mwenendo wa maisha uko kila mahala. Kutokana na mahitaji ya maisha, kuna idadi kubwa ya watu ambao neva zao hazitulii. 

Kulala ni moja ya tiba za mwili. Usingizi husaga chakula na huondoa uvimbe katika tumbo, udhaifu na uchovu.

Kukesha usiku kucha husababisha kutosagika kwa chakula tumboni na hudhoofisha akili na pia husababisha akili kuvurugika. Kulala huleta pumziko kamilifu la mwili na akili. 

Madaktari wetu wanasema kuwa, kulala ni muda ambao metaboliki ya mwili hufanyika polepole kiasi kwamba sehemu kubwa ya vyanzo vyake vya nishati hupatikana kwa ajili ya makuzi ya afya njema ya mwili na akili. 

Sehemu ya kulala inatakiwa iwe ni tulivu na isiyo na kelele, pia iwe na hewa safi na asilia. Hewa asilia ina athari nzuri katika mwili wa mwanadamu, miongoni mwa athari zake ni kuiwezesha akili kufanya kazi barabara, na pia huongeza hamu ya kula. 

Kiwango cha wastani cha kulala kinachotakiwa hutegemeana na umri. Katika umri wa miaka miwili, mtu hushauriwa kulala saa 14 hadi 16 kwa siku. Miaka minne saa 12-14 kwa siku, miaka sita hadi minane saa 11-12 kwa siku, miaka minane hadi 11 saa 10-11 kwa siku, miaka 14 hadi 18 saa 8-9 kwa siku. Watu wazima wanahitaji saa za kulala kati ya sita na nane. 

http://pendo.proboards.com/index.cgi?board=healthafya&action=display&thread=34

Mambo Muhimu Ya Kufahamu Kuhusu Ukimwi

Maana ya Neno UKIMWI 

Neno UKIMWI ni kifupisho cha maneno Upungufu wa Kinga Mwilini. UKIMWI ni mkusanyiko wa magonjwa yanayotokana na kudhoofika kwa nguvu ya mwili kujikinga na magonjwa kunakosababishwa na Virusi Vya UKIMWI (VVU). 

Maana ya neno Virusi Vya UKIMWI (VVU)

Virusi Vya UKIMWI (VVU) ni vimelea vidogo vidogo vinavyodhoofisha na kufanya mwili kupoteza uwezo wa kupambana na magonjwa. Kawaida miili yetu hukingwa dhidi ya maradhi na chembechembe nyeupe za damu, lakini VVU vikiingia mwilini hushambulia chembechembe hizo na kuzipunguza. Hivyo, mwili ulioingiliwa na VVU hupungukiwa sana na chembechembe nyeupe na hukosa kinga dhidi ya maradhi. Ingawaje mara nyingi maneno haya yamekuwa yakitumika pamoja, ieleweke kwamba yana maana tofauti.

Jinsi Virusi Vya UKIMWI Vinavyoambukizwa 

Virusi Vya UKIMWI vinapatikana katika damu na majimaji mbalimbali yanayotoka kwenye mwili na viungo vya uzazi vya wanawake na wanaume wenye uambukizo. Njia kuu ya kueneza virusi hivi, hasa katika Bara la Afrika ni kujamiiana kusiko salama. Njia nyingine ni kutoka kwa mama mjamzito
mwenye Virusi Vya Ukimwi kumwambukiza mtoto wakati akiwa tumboni, anapozaliwa au wakati wa kumyonyesha. VVU pia huambukizwa kwa kuongezewa damu yenye virusi hivyo. Pia ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kwa kuchangia vifaa vyenye mabaki ya damu kama sindano, mikasi, wembe, mipira ya kutolea mkojo au vifaa vya kutogea masikio. 

Njia zifuatazo haziambukizi VVU 

  • Kushikana mikono na mtu mwenye VVU 
  • Kubadilishana nguo na mtu mwenye VVU ili mradi hazina majimaji au damu kutoka kwa mgonjwa wa UKIMWI 
  • Kuishi pamoja na mtu mwenye VVU 
  • Kushiriki kula chakula pamoja na mtu mwenye VVU 
  • Kugusana au kukumbatiana na mtu mwenye VVU 
  • Kushirikiana bafu na mtu mwenye VVU  
  • Kuumwa na mbu, viroboto, au wadudu wengine. 

Njia hizo zilizoorodheshwa hapo juu zisihusishe damu au majimaii mengine kutoka kwa mgonjwa wa UKIMWI 

Dalili za UKIMWI  

Hakuna njia ya hakika ya kumtambua mtu aliyeambukizwa VVU zaidi ya vipimo vya maabara. Watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI wanaweza kuonekana wazima na wasionyeshe dalili zozote za ugonjwa.  Hata hivyo pamoja na kutokuonyesha dalili zozote, mtu huyu mwenye virusi anaweza akaambukiza watu wengine ikiwa atakuwa na mahusiano yasiyo salama. 

UKIMWI ni hatua ya mwisho ya maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.  Hatua hii ikifikiwa mwathirika huanza kushambuliwa na magonjwa mbalimbali yaitwayo magonjwa nyemelezi Dalili za UKIMWI zimegawanyika katika makundi mawili makuu:

Dalili kuu za UKIMWI 

•Kupungua uzito asilimia 10 au zaidi katika mwezi mmoja, bila sababu inayoeleweka 
•Kuharisha kwa muda mrefu  (mwezi mmoja au zaidi) 
•Homa kwa mwezi mmoja au zaidi

Dalili Ndogo za UKIMWI Utando mweupe mdomoni

•Kikohozi kwa muda wa mwezi mmoja au zaidi 
•Kupata mkanda wa jeshi (moto wa Mungu)
•Vipele sugu na vyenye kuwasha hasa mikononi na miguuni

Mgonjwa akiwa na dalili kuu tatu, au mbili kuu na ndogo mbili uwezekano wa kuwa na UKIMWI ni mkubwa. Hata hivyo vipimo zaidi vya maabara vinahitajika ili kuthibitisha kama mgonjwa ana UKIMWI.

Ugonjwa wa Hemoroid (HAENORRHOIDS) na kutokwa damu njia ya haja kubwa

TATIZO hili hujulikana pia kama ugonjwa wa vifundo katika njia ya haja kubwa. Jina jingine la ugonjwa huu ni bawasili, lakini kwa daktari bingwa wa upasuaji humaanisha matatizo katika mishipa ya damu (veins) katika njia ya haja kubwa (rectum or anus).

Hutokana na kulegea kwa misuli laini ya mishipa hiyo ya damu, hivyo mishipa kutanuka kuliko kawaida na kulegea, kisha kutokeza katika njia ya haja kubwa, ikiambatana na ukuta wa njia hiyo.

Sababu hasa ya kulegea kwa mishipa hiyo haijaweza kueleweka, lakini mabadiliko yafuatayo huchangia kwa kiasi mkikubwa.

•Kupata choo kigumu mara kwa mara

•Kuharisha mara kwa mara

•Kukaa kwa muda mrefu

•Kuwa na uzito mkubwa kuliko inavyotakiwa (BMI>30)

•Kukohoa mara kwa mara

•Uvimbe tumboni

•Kuzaa watoto wenye uzito mkubwa mfano zaidi ya kilo 4

Dalili

Kuhisi kushuka kwa fundo la sehemu ya haja kubwa wakati wa kupata choo, ambalo linaweza kurudi lenyewe ndani, baada ya kupata choo au inabidi kulirudisha kwa kidole au kushindikana kabisa kurudishwa kidole na kubaki likininng’inia nje kwa muda mrefu.

Kutokwa damu wakati wa haja kubwa ambayo huweza kuchafua nduo za ndani, wakati mwingine damu hutoka kwa wingi na mfululizo bila kuganda, hivyo kuhatarisha maisha.

Kuchafua nguo za ndani kutokana na kutokwa na majimaji sehemu za hajakubwa

Dalili nyingine ni kupatwa na maumivu makali sehemu za hajakubwa, fundo kuwa kubwa sana na kubadilika rangi, wakati damu inapokuwa imeganda ndani ya mishipa yake (thombosed prolapsed haemorrhoids)

Uchunguzi na matibabu

Ni vyema uonapo dalili hizo hapo juu uende katika hospitali iliyo karibu na kupata ushauri na matibabu ya kitaalamu zaidi.

Ni rahisi zaidi kwa daktari kuchunguza na mara moja kugundua ugojwa huu na ukubwa wa tatizo, pia kupanga njia ya matibabu. Pia lazima kuanza na vipimo vya mwanzo, mfano kupima wingi wa damu, (hemoglobin level)

Vipimo kama proctoscopy (kuchuguza kwa chombo maalumu chenye mwanga), proctosigmoidoscopy huweza kufanyika, pia kuwekewa dawa maalumu, kisha kupiga ex-ray (barium enema)

Kwa watu walio na umri mkubwa, mfano miaka 50 na zaidi ni muhimu kuchunguzwa kitaalamu zaidi, maana kundi hili lina hatari ya kupata saratani ya njia ya haja kubwa.

Hivyo, mtu anaweza kufikiri ni tatizo dogo, kumbe anasumbuliwa na saratani ya njia ya haja kubwa na hivyo matibabu hubadilika.

Ugojwa huu pia unaweza kuchanganywa na wa kushuka kwa sehemu ya utumbo na kutokeza nje ya njia ya haja kubwa (rectal prolapsed)

Matibabu

Iwapo hemoroid hazijawa kubwa sana, yaani zipo katika hatua ya kwanza au ya pili hivi, basi ni muhimu kukwepa au kutibu visababishi vinavyochochea ugonjwa kama vilivyoainishwa hapo juu. Mfano choo kigumu na kadhalika. Pia mgonjwa huweza kupewa dawa ya kulainisha sehemu ya haja kubwa.

Iwapo tatizo ni kubwa yaani lipo katika hatua ya tatu au ya nne, au matibabu tajwa hapo juu yameshindikana, basi upasuaji ndiyo matibabu sahihi ya ugonjwa huu. Upasuaji mzuri huo upo wa aina nyingi, mfano kukata au kuvifunga vifundo kwa mpira maalumu. Ifahamike kwamba mgonjwa anapokuja katika hali hatarishi kama vile vifundo kuwa na maumivu makali na kutoka damu kwa wingi (thombosed and prolapsed hemorrhoids), basi huhitajika kufanyiwa upasuaji mapema ili kumwokoa mgojwa.

Matatizo yatokanayo na ugonjwa huu

Yapo mengi, lakini kwa uchache ni kama;

•Kushindwa kupata haja kubwa katika hali ya kawaida kutokana na kupata maumivu

•Choo kuwa kigumu zaidi jinsi muda unavyokwenda na hivyo kuongeza ukubwa wa tatizo

•Kutokwa damu wakati wa kujisaidia haja kubwa

•Kutokwa damu nyingi pale hemoroidi zainapopasuka hivyo kuhatarisha maisha ya mgonjwa

•Kuchafua nguo na kuleta adha katika jumuiya mfano kazini na majirani.

Kwa Mawasiliano 0754310407 

http://www.mwananchi.co.tz/Makala/-/1597592/1691234/-/item/0/-/h54mot/-/index.html